Je Wajua? - Wakulima Wa Miwa Wana Njia Ya Kidemokrasia Ya Kuchagua Wawakilishi Wao Katika Bodi Ya Sukari Ya Kenya

Je Wajua? - Wakulima Wa Miwa Wana Njia Ya Kidemokrasia Ya Kuchagua Wawakilishi Wao Katika Bodi Ya Sukari Ya Kenya

Mwandishi: Etherly Barasa 

Imetafsiriwa na: Mercy Sasala

Tarehe ni tano Septemba mwaka wa 2026 — Kura Yako, Sauti Yako, Sekta Yako.

Uchaguzi wa wawakilishi wa wakulima wa miwa katika Bodi ya Sukari Kenya (KSB) umekaribia. 

Kwa kila mkulima aliyesajiliwa na kuthibitishwa, huu ni wakati muhimu wa kuelewa uchaguzi huu unahusu nini, kwa nini ni muhimu na jinsi ya kushiriki. 

Tofauti na bodi nyingi za mashirika ya umma ambapo wajumbe wengi huteuliwa, wakulima wa miwa wana fursa maalum ya kuwachagua wawakilishi wao katika Bodi ya Sukari Kenya. Chini ya Sheria ya Sukari ya mwaka 2024, wakulima watachagua wawakilishi watano, mmoja kutoka kila mojawapo ya maeneo matano ya kilimo cha miwa nchini. 

KWA NINI UCHAGUZI HUU NI MUHIMU KWA MKULIMA? 

Mwakilishi wa mkulima si jina tu kwenye bodi. Ni sauti ya wakulima katika meza ya maamuzi. 

Kupitia mwakilishi wao, wakulima wanaweza kuwasilisha changamoto na masuala yanayowakabili, kama vile: 

  • Malipo ya haki na kwa wakati kwa miwa iliyowasilishwa. 
  • Kuboresha miundombinu katika maeneo yanayolima miwa. 
  • Huduma na usaidizi bora kwa wakulima. 
  • Sera na maamuzi yanayolinda maslahi na ustawi wa wakulima. 

Mwakilishi anatarajiwa kuwasilisha maoni, changamoto na mapendekezo ya wakulima wa eneo lake kwa Bodi, na kutetea maslahi yao bila kuathiriwa na vitisho au ushawishi usiofaa kutoka kwa wamiliki wa viwanda au serikali. 

Kwa hiyo, uchaguzi huu si tu kuhusu kuchagua mwakilishi. Ni njia ya wakulima kushiriki katika maamuzi yanayoathiri maisha yao na mustakabali wa sekta ya sukari. 

UCHAGUZI HUFANYIKAJE? 

Mchakato wa uchaguzi huanza kabla ya siku ya kupiga kura. 

Bodi ya Sukari Kenya ilishirikiana na wamiliki wa viwanda na vyama vya wakulima kupata sajili zilizokuwepo za wakulima. Sajili hizo ziliunganishwa na kufanyiwa uhakiki ili kuunda sajili pana zaidi ya wapiga kura. 

Katika zoezi la usajili na uhakiki lililofanyika tarehe 25 Mei hadi tarehe 4 Juni 2026, wakulima walipata nafasi ya kuthibitisha wasifu wao na kujulishwa vituo vyao vya kupigia kura kulingana na maeneo yao ya kilimo cha miwa. 

Baada ya kuzingatia idadi ya wakulima, maeneo wanamoishi, umbali, na hali ya kijiografia, Bodi ilibainisha vituo mia sita sitini na nane (668) vya kupigia kura katika maeneo matano ya kilimo cha miwa. 

Bodi pia ilifanya kampeni za uhamasishaji kupitia redio, misafara ya uhamasishaji, vipeperushi, na njia nyingine za mawasiliano ili kuwafikia wakulima. 

NANI ANAYESTAHILI KUPIGA KURA? 

Kuishi katika eneo linalolima miwa pekee hakukufanyi uwe mpiga kura. 

Ili kupiga kura, ni lazima uwe: 

  • Mkulima wa miwa aliyesajiliwa na kuthibitishwa 
  • Jina lako liwe katika sajili ya wapiga kura ya eneo lako husika; na 
  • Uwe na nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya utambulisho na uthibitishaji. 

Katika usajili wa wakulima uliofanyika, wakulima walitakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (ID) au pasipoti, pamoja na ushahidi wa malipo ya miwa, taarifa ya ugavi wa miwa au kibali halali kinachohusiana na kipindi kinachohitajika. 

Masharti maalum yalitumika kwa eneo la Pwani. 

Usajili na uhakiki wa taarifa ni muhimu ili kukuwezesha kushiriki katika uchaguzi. 

NANI ANAWEZA KUWANIA NAFASI YA MWAKILISHI WA WAKULIMA? 

Masharti ya kuwa mgombea ni magumu zaidi kuliko yale ya mpiga kura wa kawaida. 

Miongoni mwa masharti muhimu ni kwamba mgombea: 

  • Awe mkulima hai wa miwa katika eneo husika. 
  • Awe amekuwa mkulima katika kipindi kinachohitajika cha miezi 24 (miaka miwili) iliyopita, isipokuwa kwa masharti maalum ya Pwani. 
  • Awe na mkataba halali wa kusambaza miwa au taarifa ya ugavi kutoka kwa kiwanda katika eneo lake husika. 
  • Awe amewasilisha angalau tani hamsini (50 tons) za miwa kutoka shamba lake kwa kiwanda katika kipindi kinachohitajika (miaka miwili), isipokuwa kwa masharti maalum ya Pwani. 
  • Awe raia wa Kenya na awe na angalau elimu ya Kidato cha Nne. 
  • Atimize masharti ya uongozi na uadilifu chini ya Sura ya Sita ya Katiba. 
  • Asiwe mfanyakazi wa Bodi ya Sukari Kenya au kiwanda cha sukari. 
  • Asiwe na wadhifa wa kisiasa wa kuchaguliwa au kuteuliwa. 
  • Asiwe mfilisi ambaye hajakamilisha masharti ya ufilisi. 
  • Awe mtu mzima mwenye akili timamu. 
  • Alipie ada ya uteuzi isiyorejeshwa ya shilingi elfu kumi (KSh 10,000). 
  • Awanie kura katika eneo moja pekee. 

 

Mgombea pia anatakiwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika, zikiwemo kitambulisho, taarifa za uwasilishaji wa miwa, vyeti vya elimu, Cheti cha ulipaji kura (KRA Tax Compliance Certificate), Cheti cha maadili mema cha polisi (Police Clearance Certificate), EACC Self-Declaration na cheti kutoka Credit Reference Bureau (CRB). 

SIKU YA UCHAGUZI — 5 SEPTEMBA 2026 

Uchaguzi umepangwa kufanyika Jumamosi, tarehe 5 Septemba 2026, kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi na moja jioni (7:00 a.m.–5:00 p.m.) katika vituo vilivyoteuliwa. 

Ikiwa wewe ni mpiga kura aliyesajiliwa na kuthibitishwa: 

Jua kituo chako cha kupigia kura, beba kitambulisho chako na nyaraka zinazohitajika, na usikose kutumia haki yako ya kupiga kura. 

Upigaji kura utafanyika kwa kura ya siri, kwa kuzingatia kanuni ya mkulima mmoja, kura moja. 

Baada ya upigaji kura kufungwa, kura zitahesabiwa katika vituo husika na matokeo kujumlishwa katika ngazi ya eneo la kilimo cha miwa. Mgombea anayepata kura nyingi zaidi katika kila eneo ndiye atakayekuwa mwakilishi wa wakulima wa eneo hilo, kulingana na taratibu za kisheria za kuthibitisha na kumteua mwakilishi. 

NINI KITAFANYIKA IWAPO KUNA MGOGORO? 

Utaratibu wa uchaguzi umeweka Kamati ya Kutatua Migogoro ya Uchaguzi kushughulikia malalamishi yanayohusiana na mchakato wa uchaguzi. 

Malalamiko kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi ndani ya saa ishirini na nne (24hrs) baada ya kutangazwa kwa orodha ya wagombea walioteuliwa, pamoja na ushahidi unaohitajika, na ada isiyorejeshwa ya shilling elfu tano (KSh 5,000). 

Malalamishi ya siku ya uchaguzi yanapaswa kuwasilishwa kwanza kwa Afisa Mkuu wa Kituo cha Kupigia Kura (Presiding Officer). Ikiwa hayatatatuliwa, yanaweza kuwasilishwa kwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi (Chairperson of elections Committee) kwa hatua zaidi. 

MWAKILISHI ATAHUDUMU KWA MUDA GANI? 

Mwakilishi wa wakulima atahudumu kwa muda wa miaka mitatu kwenye bodi. Sheria pia inaweka vipindi tofauti vya kumalizika kwa mihula ya wajumbe mbalimbali wa Bodi, kumaanisha sio lazima Bodi nzima ibadilishwe kwa wakati mmoja. 

HITIMISHO. 

Uchaguzi wa mwakilishi wa wakulima ni zaidi ya kuchagua mtu wa kuketi kwenye Bodi. Ni fursa ya mkulima kushiriki moja kwa moja katika maamuzi yanayohusu maslahi yake na mustakabali wa sekta ya sukari nchini. 

Ikiwa wewe ni mkulima aliyesajiliwa na kuthibitishwa, fahamu kituo chako cha kupigia kura, beba kitambulisho chako na ushiriki katika uchaguzi. 

KUMBUKA, TAREHE NI TANO, MWEZI WA SEPTEMBA, MWAKA WA 2026 

KURA YAKO. SAUTI YAKO. SEKTA YAKO. 

Share this Post: