Mwandishi: Mercy Sasala
Na je, wajua kua ubora wa miwa haupimwi kwa uzito wake pekee?
Chukua mfano wa hali ambayo wakulima wawili wameleta tani moja ya miwa kila mmoja. Kwa macho, wanaweza onekana kuwa wameleta kiasi sawa cha zao. Lakini je, miwa hiyo ina kiwango sawa cha sukari? Je, yote imevunwa kwa wakati unaofaa? Na je, kila tani itatoa kiasi sawa cha sukari inapofikishwa kiwandani?
Yapaswa kufahamu kwamba, kila tani ya miwa inayovunwa hutofautiana katika ubora. Tofauti hio hutokana na jinsi mkulima alivyo shughulikia miwa yake shambani. Kwanzia kuchagua mbegu, hadi kuvuna.
Ubora wa miwa hujulikana kwa njia gani?
Uchambuzi wa miwa unahitaji usahihi, vifaa vya kisasa na wafanyikazi waliofunzwa na kufuzu. Hapa ndipo Kitengo cha Kupima Miwa cha Bodi ya sukari ya Kenya, yaani CTU kinapoingilia kati.
Kabla ya miwa kuingia kiwandani, maabara za huduma za upimaji wa miwa hufanya kazi muhimu ya kuchukua sampuli na kuipima.
Kwanza, sampuli ndogo inayowakilisha miwa yote kwenye tinga au lori inachukuliwa.
Kisha, sampuli hiyo inasagwa vizuri na inapimwa kwa mashine maalum (NIR Spectrometer) ili kubaini viashiria muhimu vya ubora wa miwa, ikiwemo kiasi cha unyevunyevu (moisture), kiasi cha nyuzi ya miwa (fibre) na kiasi cha sukari kwenye miwa (pol/sucrose).
Kwa nini vipimo hivi? Kwa sababu, sio sukari pekee tunayopata kwenye miwa bali pia molasi (molasses), na mabaki ya nyuzi ya miwa yaani bagasse yanayotumika kwa uzalishaji wa umeme.
Utapata maelezo zaidi kuhusu huduma za upimaji wa miwa (cane testing services) chini ya ukurasa wa App ya Miwa Bora, sehemu lililoandikwa “MORE”.
Ni nini umuhimu wa kupima ubora wa miwa?
Kwa miaka mingi, mkulima wa miwa amekuwa akilipwa kwa kuzingatia tu uzito wa miwa yake.
Lakini kumbuka kuwa, wakulima wanatofautiana kwa jinsi walivyo kuza mimea yao na aina ya mbegu ya miwa waliyopanda. Hii inamaana kuwa, ingawa miwa yaweza kua na uzito sawa, kiasi cha sukari kwenye miwa hio kinaweza kuwa tofauti.
Hili ndilo wazo lililo zalisha mfumo wa malipo ya miwa kwa kuzingatia ubora wake, yani QBCPS (Quality Based Cane Payment System).
Mfumo huu uliundwa ili kuongoza sekta ya sukari nchini kwenye mwelekeo wa kumlipa mkulima kwa ubora wa miwa, sio kwa uzito tu. Chini ya QBCPS, data za ubora wa miwa, hasaa kiwango cha sukari (sucrose) kitatumika kubaini thamani ya miwa inayoletwa viwandani.
Mkulima atafaidika vipi katika mfumo huu wa malipo?
Jibu ni rahisi. MIWA BORA → MALIPO ZAIDI!
Mkulima anatakiwa kufanya nini ili kupata miwa yenye ubora wa hali ya juu?
-
Kuchagua aina ya mbegu za miwa zilizothibitishwa na zenye sukari nyingi (high sucrose).
-
Kuvuna miwa wakati wa ukomavu unaofaa.
-
Kuboresha usimamizi wa shamba kama vile kupalilia wakati unaofaa na kutumia mbinu kama vile umwagiliaji maji kwenye miwa wakati wa ukame.
-
Kuzingatia zaidi mbinu bora za kuvuna na kuepuka kukata muwa juu sana (high cutting) wakati wa kuvuna.
Kwa ufupi, QBCPS inalenga kuwapa wakulima motisha ya kuzalisha miwa yenye ubora wa hali ya juu, kuimarisha uwazi kwa malipo, na kumtuza mkulima kwa bidii aliyofanya shambani mwake.
